Muungano wa Kenya Kwanza unaongozwa na naibu Rais Dkt.William Ruto umeahidi kufufua sekta za kilimo na utengenezaji bidhaa katika kaunti ya Kiambu.
Akihutubia kongamano la kiuchumi katika jumba la mikutano la Jumuia mjini Kiambu Jumatatu asubuhi, Naibu huyo wa Rais, alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe tisa mwezi Agosi mwaka huu, atapea kipaumbele ufugaji wa ng’ombe wa maziwa katika kaunti hiyo ambayo inafahamika kuwa moja ya kaunti zinazozalisha maziwa kwa wingi humu nchini kwa kupunguza gharama ya lishe za mifugo.
Alitaja ukuzaji wa Sim sim, Soya na malighafi nyingine zinazohitajika kwa uzalishaji wa lishe za mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanapata lishe hizo kwa bei nafuu.
Aidha Dkt. Ruto pia alitoa ahadi ya kusaidia vyama vya ushirika vya wakulima wa kaunti hiyo katika kujenga viwanda vya utayarishaji bidhaa.
Ruto ameahidi kuhahakikisha wakulima wanafahamishwa kuhusu kiwango cha chini cha faida watakayopata, ili kuhakikisha wakulima wanajua bei za mazao yao kabla ya kuyauza.
Naibu rais alikuwa akijibu malalamishi ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika kaunti ya Kiambu waliosikitika kutokana na kiwango cha chini cha maziwa na bei za juu za lishe za mifugo.